Monday, 29 October 2018

DHANA YA MOFU




 
 DHANA YA MOFU NA AINA ZAKE

TUKI(1990), katika Dafina ya Lugha wanasema kuwa, “Mofu ni kipashio cha isimu maumbo kiwakilishacho mofimu”.
Massamba (2004), katika Dafina ya Lugha anasema , Mofu ni kipashio cha kimaumbo ambacho huwakilisha mofimu.
Kwa mujibu wa Nida (1949), wanasema, Mofu ni umbo la neno ambalo huwakilisha mofimu na ambalo huthihirika kifonolojia na kiothografia.
Mofu ni kipashio kidogo kabisa chenye maana katika lugha.Mofu hawezi kugawanywa katika sehemu ndogo zaidi bila kuharibu maana yake. Mofu huwakilisha maana za kileksika na zile za kisarufi. (Platt,1985).
Kwa ujumla, Mofu ni kipashio cha kimofolojia ambacho husitiri maana za mofimu katika lugha na huweza kudhihilika kifonolojia zinapotamkwa na kiothografia zinapoandikwa katika lugha.
Mofu huainishwa kwa kuzingatia vigezo viwili; Kigezo cha maana zinazowakilishwa na mofu na Kigezo cha mofolojia ya mofu.
Tunapotumia kigezo cha maana zinazowakilishwa na mofu, tunapata aina tatu za mofu, yaani; mofu huru/sahili, mofu funge na mofu tata,kwa upande mwingine tunapotumia kigezo cha mofolojia au maumbo ya mofu zenyewe tunapata aina mbili za mofu, yaani; mofu changamano na mofu kapa. Hivyo, kwa kuanza na kigezo cha maana zifuatazo ni aina za mofu;
 Mofu huru/sahiliMofu huru ni zile mofu ambazo zinaweza kukaa peke yake kama maneno kamili yenye maana inayoweza kueleweka bila kusaidiwa na mofu nyingine. Aghalabu, mifano mingi ya mofu huru hupatikana kutoka kwenye vipashio vya lugha, kama ifuatavyo:
-Nomino:  {baba}, {kuku}, {sungura}, {ndege}, {dada}, {paka}.
-Vivumishi: {safi}, {baya}, {dhaifu}, {zuri}, {imara}, {hodari}.
-Viwakilishi:{mimi}, {sisi}, {wewe}, {ninyi}, {yeye), {wao}.
-Vielezi:  {upesi}, {haraka}, {sana}, {leo}, {jana}, {juzi}.
-Vitenzi: {tafiti}, {samehe}, {arifu}, {sali}, {jibu}, {badili}.
-Viunganishi:{na},{halafu}, {bado}, {ila}, {aidha},{pia}.
Kwa hiyo, Kiswahili kinazo mofu huru/sahili nyingi ambazo zimo katika aina karibu zote za maneno(vipashio) za lugha. Hivyo, mofu huru ni mofu ambazo zinaweza kukaa peke yake kama maneno kamili yanayoeleweka bila kusaidiwa na viambishi.
 Mofu funge/tegemeziMofu funge au Mofu tegemezi ni mofu ambayo haiwezi kutumiwa peke yake kama neno lililo na maana yake kamili; aghalabu mofu funge hutumiwa kama kiambishi tu kinachoambatanishwa na mzizi au viambishi vingine ili kulikamilisha neno husika. Mofu funge ina sifa zake ambazo ni pamoja na;
-Mofu funge haiwezi kukaa peke yake ikawa neno kamili.
-Mofu funge ni lazima iambatanishwe na angalau mafu nyingine moja ndipo tupate neno
kamili. 
Mifano ya Mofu funge/tegemezi ni kama ifuatayo;
Idadi ya Umoja       Idadi ya Uwingi
m-toto (m)                 wa-toto (wa)
ki-su (ki)                    vi-su (vi)
m-ti (m)                      mi-ti (mi)
Ukumbwa wa Nomino        Udogo wa Nomino
ji-tu (ji)                                  ki-ji-tu (ki)
ji-su (ji)                                  ki-ji-su (ki)
Maana za mofu funge hutegemea sana muktadha wa mofu husika. Mofu funge ikiondolewa kwenye muktadha wake hukosa maana na ni vigumu kujua maana yake bila kuiweka katika muktadha wa neno. Mofu funge inaponing’inizwa peke yake haituwezeshi hata kidogo kujua maana yake. Umbo moja linaweza kuwa na maana nyingi kwa mujibu wa miktadha ambamo imeambatanishwa katika mzizi wa neno.
Aghalabu, mofu funge ni sawa na viambishi vya mizizi mbalimbali katika neno. Hii ina maana kwamba viambishi vilivyo vingi katika lugha huwa ni mofu funge. Tunasema viambishi vingi kwa sababu si viambishi vyote ambavyo huundwa kwa mofu funge.Yapo maneno mengine ambayo ni mofu huru. Baadhi ya mizizi ya maneno pia huwa ni ya mofu funge kwa sababu mizizi hiyo huwa haiwezi kukaa peke yake ikawa neno kamili. Mifano mizuri ya mizizi ya maneno ya Kiswahili ambayo huundwa kwa mofu funge ni ile ya vitenzi vya silabi moja moja,kama ifuatavyo:
Mfano (i): Mizizi ya maneno yenye silabi moja.
Mofu funge               Neno                   
{-l-}             kula 
{-f-} kufa
{-nyw-}       kunywa   
(ii): Mizizi ya maneno yenye silabi nyingi.
Mofu funge Neno
{-chez-} cheza
{-lim-} lima
{-sem-} sema
 Mofu Tata ,Mofu tata ni mofu ambazo huwa na maana zaidi ya moja au kuanzia mbili na kuendelea. Mfano, Ntomoka alimpigia Malamla mpira.
Sentensi hii ni tata kwa sababu ina maana zaidi ya moja.  Utata wa sentensi hii haupo kwenye muundo wake wa kisarufi, bali upo katika kitenzi alimpigia.  Kitenzi hiki kina mofu sita, yaani:
{a-} + {-li-}  + {-m-} + {-pig-} +  {-i-}   + {-a}
   1           2             3            4             5           6
Kati ya mofu hizi zote sita, mofu ya tano {-i-} ndiyo yenye utata. Mofu {i} ni mofu ya kutendea kwa sababu tukisema: ‘Ntomokaalimpigia Malamla mpira’, maana zinazoweza kueleweka na wasikilizaji ni nne:
 (a)   Ntomoka aliupiga mpira kwa niaba ya Malamla; yaani Malamla ndiye aliyetakiwa aupige mpira ule, lakini kwa sababu ambazo hazikuelezwa, badala ya Malamla kuupiga mpira ule, Ntomoka akaupiga.
(b)    Ntomoka aliupiga mpira kuelekea kwa Malamla; yaani Ntomoka na Malamla walikuwa wakicheza mpira. Ikapatikana fursa, Ntomoka akaupiga mpira ule kuelekea kwa Malamla. Kwa hiyo, hapa tunazungumzia mwelekeo wa mpira.
(c)    Ntomoka alimpiga Malamla kwa kuutumia mpira; yaani, Ntomoka anautumia mpira kama ala (silaha) ya kumpigia Malamla.
  (d)  Ntomoka alimpiga Malamla kwa sababu ya mpira; yaani hapa, mpira ndio sababu kubwa ya Ntomoka kumpiga Malamla. Tuseme labda Ntomoka alikuwa na mpira wake, halafu Malamka akauchukuwa kuuchezea na kwa bahati mbaya akaupoteza. Ntomoka anapogundua kwamba Malamla ameupoteza mpira wake, basi ndipo akampiga.
Kwa maelezo hayo, ni wazi kwamba sentensi yetu ina utata kwa kuwa inatupatia maana tofauti tofauti zipatazo nne ambazo zimesababishwa na mofu {-i-} ya kutendea.
Kwa kutumia kigezo cha mofolojia au maumbo ya mofu zenyewe, zifuatazo ni aina za mofu;
Mofu ChangamaniMofu changamani ni mofu ambazo huundwa kwa kuweka pamoja angalau mofu huru mbili au mofu funge na mofu huru na kuunda neno lenye kuleta maana kamili, kwa mfano:
Mofu huru + Mofu huru
- {fundi}  +  {chuma} = fundichuma.                     
- {gari} +  {moshi} =  garimoshi.
Mofu funge + Mofu huru
-{mw} + {ana} + nchi = mwananchi. 
  • {ki} + {ona} + mbali = kionambali.
Mofu KapaMofu kapa ni mofu za pekee ambazo hazina umbo. Mofu kapa hazitamkwi wala kuandikwa. Mofu kapa hazionekani katika neno, lakini athari zinazotokana na hiyo mofu kapa husika hueleweka. Ingawa mofu hizi huwa hatuzioni wala kuzitamka au kuziandika, lakini maana zake tunazipata. Nomino za Kiswahili zinaweza kugawanywa katika makundi mbalimbali kulingana na maumbo yake ya umoja na wingi kama ifuatavyo;
=Nomino zilizo na kiambishi awali cha umoja tu, cha wingi ni kapa  (ø)
Mfano:          
            Umoja                        Wingi
- kuta                       Ã¸ - kuta
            - funguo                  Ã¸ - funguo
            – kucha                    Ã¸- kucha.
        
- Nomino zilizo na kiambishi cha wingi tu, cha umoja ni kapa  (ø)
Mfano:
            Umoja                        Wingi
           Ã¸ -kasha                 ma – kasha.
           Ã¸ -debe                    ma – debe.
ø-jembe                 ma – jembe
-Nomino zisizo na kiambishi cha umbo la umoja wala wingi.(ø)
Mfano;
Umoja Wingi
ø -mama Ã¸-mama
ø-mbuzi Ã¸-mbuzi
ø-manukato Ã¸-manukato
 Sherehe kuhusu mofu kapa.Kinachotokea hapa ni kwamba ukisema ukucha watu wanaelewa kuwa ni ukucha mmoja tu. Lakini ukisema kucha,  watu wataelewa kuwa ni kucha nyingi.Na hali hii ndivyo ilivyo kwa maneno ufunguo – funguo, ukuta - kuta, inajulikana kuwa ni ufunguo mmoja tu na akisema funguo, ni kwa maana ya wingi lakini umbo  lenyewe linaloileta hiyo maana ya wingi halionekani bayana katika neno.
Ili kuyaeleza haya maumbo ambayo hayapo lakini maana zinazowakilishwa na maumbo hayo zipo, Wanaisimu wamekubaliana kuyaita maumbo  haya kapa, yaani mofu ambazo hazipo. Mofu hizi ni   dhahania tu katika akili zetu kwa kufahamu tu kwamba maana fulani haiwezi kuja tu yenyewe lazima iletwe na mofu fulani. Kwa hivyo, hata kama mofu hiyo haionekani, lakini ipo ni mofu-kapa.
Kwa kuhitimisha, mofu ni umbo muhimu sana katika lugha kwani kupitia maumbo haya ndipo tunaweza kuelewa maana mbalimbali za vitamkwa katika neno kidhahania yaani mofimu, hata mzizi pia ni mofu. Kila lugha ina mofu zake mfano lugha ya kiingereza, Kiswahili na hata lugha za kibantu.

MAREJELEO
Maganga (1997), OSW 102: Historia ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Masebo, J. A. Nyengwine, N. (2002), Nadharia ya Lugha ya Kiswahili, Kidato cha
5na6.  Aroplus Industries Ltd: Dar es Salaam.
Nkwera, Fr. F. V. (2003), Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu, Sekondari na Vyuo.
Creative Prints Ltd: Dar es Salaam.
Matinde, S.R.(2012), Dafina ya Lugha, Isimu na Nadharia.Mwanza: Serengeti
Educational Publishers.
TUKI. (2014).Kamusi ya Kiswahili Sanifu,Nairobi:Oxford university press.

DHANA YA VITAMKWA



UTANGULIZI
Vitamkwa, ni neno linalotokana na kitenzi ‘Tamka’ ambalo lina maana ya kitendo cha kutoa nje ye kinywa au pua ya mwanadamu sauti ambazo hutumika katika mazungumzo au usemi wowote uwao. (Kihole, Masamba na Hokororo, 2003).
Hivyo basi, vitamkwa ni sauti ambazo hutolewa na binadamu kupitia katika chemba ya kinywa na chemba za pua  kwa kufuata utaratibu maalumu. Utaratibu huu huhusu namna au jinsi ya kuzitoa sauti hizo na mahali pa kutolea sauti hizo.
Mfano:  [ p ] + midomo – mahali
               [ p ] + midomo ishikane na kuachana
Lakini pia sauti hizi zitamkwazo zaweza  kuwa ni konsonanti  na irabu (vokali).
Mfano:  [ b ], [ d ] kama konsonanti na [ e ],[ u ],[ i ] kama vokali au irabu.  
Vitamkwa, ni sauti zitumikazo katika lugha fulanina hujumuishwa kwa jina la Alfabeti ambazo ndani yake kuna konsonanti na irabu.  Mfano: a, b, c, d, e, f.
Kuna baadhi ya wataalamu mbalimbali ambao wameelezea sifa za vitamkwa na baadhi ya wataalamu hao ni pamoja na Romani Jackobson na Nikolaji Trubertzkoy.
Roman Jakobson,Ni raia wa Urusi(Russia) alizaliwa October 11,1896,Moscow na alifariki July18,1982.Cambrige alikuwa mwalimu wa Linguistic na ni mmoja wa waanzilishi wa Prague kwa kushirikiana na Halle walibainisha sifa Kinzani za lugha katika makund imawili ,Konsonanti na vokali na baadae makundi madogo manne Konsonanti halisi,Vokali,Vitambaza naViyeyusho kwa kutumia Nadharia ya Sifa Pambanuzi
Nikolaj Trubertzkoy,huyu nae ni raia wa Urusi(Russia)  Alizaliwa April,16,1890 mjini Moscow na kufariki  June,25,1938 alikuwa mwalimu wa masomo ya Historian a Kiingereza katika vyuo vikuu vya Moscow,Vienna na Sofia nchini urusi pia alikuwa mwanzilishi wa mawazo ya Prague.Mwaka 1969 alibainisha sifa za vitamkwa kwa kutumia Nadharia ya Upambanuzi au Nadharia ya Ukinzani Pambanuzi .zifuatazo ni tofauti za sifa za vitamkwa zilizoelezwa na Nikolaj Trubertzkoy na Roman Jakobson.
Trubertzkoy, alizibainisha sifa za vitamkwa kifonetiki na kifonolojia lakini alijikita zaidi katika Fonetiki kwani katika upambanuzi wake ametumia lugha mbalimbalikama; Kiingereza,Kijerumani na Kiswahili.Ilhali Jakobson alipendekeza sifa za vitamkwa kifonetiki na kifonolojia lakini alielemea zaidi katika sifa za vitamkwa kifonolojia katika lugha ya Kiswahili.Ambapo alielezea Konsonanti na Vokali za Kiswahili.
Nikolaj Trubertzkoy,ametumia Nadharia ya upambanuzi WakatiJakobson alitumia Nadharia ya Sifa Pambanuzi.
 Katika Nadharia ya Upambanuzi, Trubertzkoy madai yake ya msingi ya Nadhari yake ni kwamba pakiwa na Upambanuzi basi lazima patakuwepo na ukinzani.kwa mfano Ukinzani wa kiuwili ambapo jumla ya sifa bainifu zinazochangiwa na sauti mbili kinzani hupatikana katika sauti hizo mbili peke yake na si kwingineko.Mfano Vipasuo vya mdomo [P] na [b] katika Kiswahili ambavyo vinachangia sifa ya Vipasuo vya midomo, hakuna vipasuo vingine vinavyochangiansifa hiyo.LakiniKatika Nadharia ya Sifa Pambanuzi yake Roman Jakobson, anabainisha sifa za Kimatamshi dhidi ya Sifa Kiaukustika.Kwa mfano katika sifa za Kiaukustika anabainisha sifa ambazo ni;
Sifa ya Usononanti.
Hii ni sifa ambayo hujitokeza katika kutamka irabu na huwa na mguno mkubwa (vokali). Sifa hii ilitumiwa kubainisha sauti za konsonati na irabu. Katika ubainishaji wake, irabu ingeoneshwa kuwa na sifa ya usonoranti [ +usonoranti], lakini konsonanti ingeoneshwa kuwa si ya usonoranti [-usonoranti]. Mfano, kimadende na kitambaza /r/ na /l/ ni konsonanti lakini huwa na usonoranti [+usonoranti]. Nazali hupewa sifa ya usonoranti, /m/ na /n/ [+usonoranti], viyeyusho navyo pia hupewa sifa ya usonoranti, /w/ na /y/.  
 Sifa ya Uprotensi.
Sifa hii hutumiwa kutofautisha zile fonimu ambazo ni kaze. Sauti kaze, ni zile ambazo hutamkwa kwa kutumia nguvu nyingi na zinakaa muda mrefu zinapotamkwa. Mfano, sauti si ghuna huwa ni kaze (+kaze) Ilihali sauti si ghuna ni sauti si kaze (-kaze).
Mfano: sauti /t/ si ghuna kwa hivyo ni kaze (+kaze), fonimu /d/ ni ghuna kwa hivyo ni sauti si kaze (-kaze).
 Sifa ya Utoni
Hii ni dhana ambayo hutumiwa kuelezea uhusiano baina ya sauti mbili au zaidi za fonimu moja ambazo haziwezi kutokea katika mazingira sawa. Mfano, fonimu /k/ na /v/.
                        [k]                                    [v]
                       +Konsonanti                   +Konsonanti     
                       +Kizuiwa                        +Kikwamizwa   
                       +Kaka laini                     +Midomo meno
                       -Nazali                             -Nazali
                       -Ghuna                            +Ghuna
Katika kuzieleza sifa za Vitamkwa ,Trubertzkoy alielezea kwa kuzigawa sifa hizo katika Seti tatuza Ukinzani Pambanuzi ,seti hizo ni kama zifuatazo;
Seti ya kwanza,katika seti hii alizipambanua katika vipengele vinneambavyo ni; Ukinzani kiuwili,Ukinzani kiwingi, Ukinzani kiwiani na Ukinzani kipeke.
        i.            Ukinzani kiuwili, huu ni ukinzani ambao anaeleza kuwa Sifa mbili kinzani hupatikana katika sauti hizo mbili peke yake na si kwingineko.Mfano,vipasuo vya midomo  [P] na [b] katika Kiswahili ambavyo vinachangia sifa ya kuwa vipasuo vya kinywa vya midomo .ukinzani wake unajidhilisha katika kielelezo
            [p]                                                       [b]
+Kipasuo                                              +kipasuo
-ghuna                                                 +ghuna
      ii.            Ukinzani uwingi , ni ukinzani ambao unaeleza jumla ya sifa bainifu zinazochangiwa na sauti hizo huweza kupatikana katika seti ya sauti nyingine pia mfano herufi P na R ambazo zote zinachangia mkunjo wa upinda wa kuelekea kulia ,lakini sihizo tu balizipo na herufi nyingine kama herufi B na D ,hvyo ukinzani huo uhuhusicha herufi nyingi .
    iii.            Ukinzani kiwiani , ukinzani huu huelezae Sauti mbili zinazowiana na kukinzana na suti nyingine mbili zinazouwiana .mfano sauti [F] na [v], na ukinzana na [s] na [z] katika Kiswahili . tazama kielelezo hiki.
[f]           na         [v]                     [s]      na   [z]
        [+midomomeno ] [+midomomeno] [+ufizi]   [+ufizi].
ivUkinzani kipeke, ni ukinzani ambao ni wa kipekee kabisa. Mfano [r] na [l] kaika lugha ya kiingereza hakuna memba wengine wanaohusiana na uhusiano na wanamna hiyo . na katika lugha ya Kiswahili ukeli ni kwamba sauti [r] ni kimadende ambacho kipo peke yake pia sauti [l] ni kitambaza ambacho kipo peke yake pia .
Seti ya pili  ,katika seti hii Trubertzkoy ameigawa katika seti ndogo ndogo tatu ambazo ni seti ya kuzinzani kibinafsi, ukinzani kimwachano taratibu na ukinzani kisawa .
                    i.            Ukinzani kibinafsi , ni ukinzani ambao sauti moja inakuwa na alama ya ziada (sifa ya ziada) na suti nyingine inakuwa haina .mfano sauti moja inakuwa ghuna na nyingine inakuwa sighuna kama vile sauti [p] na sauti [b], pia sauti moja yaweza kuwa nazali na nyingine ikose sifa hiyo , kama vile sauti  [m] na [k] .
                  ii.            Ukinzani kimwachano taratibu ,ukinzani huu unaeleza kuwa memba wa seti wanapishana kwa viwango tofauti vya sauti ile ile, mfano sauti ya vokali [o] na [u] .  Tazama kielezo kifuatacho
              [o]                                      [u]
         +vokali                               +Vokali
        +Nyuma                              +Nyuma
        +Mviringo                           +Mviringo
        +Nusu juu                             +Juu 
iii Ukinzani wa kisawa, ukinzani wa memba wa kundi moja ni sawa na ukinzani baina ya kundi jingine.Kwa maana kwamba ukinzani wao si wa kupishana kwa viwango vya sifa ile ile.Mfano sauti [p]na [t],[f] na [k] katika lugha ya Kijerumani.



Seti ya tatu, hii ni seti  ambayo inaelezea  ukinzani imara  na ukinzani usio imara.Ukinzani imara ni ule ambao Usio badilifu,Mfano ni ukinzani baina ya sauti [t,d na l] ambazo zote  ni sauti za ufizi. Na  ukinzani usoimara ni ule ukinzani ulobadilifu yaani hubadilika . mfano katika mazingira ya sauti [l] hubadilika na kuwa sauti [d] katika mazingira ya kutanguliwa na Vokali [i] ,mfano  Ulimi-Ndimi.Hivyo sauti [l] si imara na sauti [d] ni imara.
Ilhali, Roman Jakobson  amependekeza sifa za vitamkwa katika makundi makuu mawili ambayo ni Kundi la sauti za Konsonanti na Kundi la sauti za vokali. Ambayo pia aliyagawa katika ,makundi madogo madogo manne.ambayo ni Konsonanti halisi,Vokali,Vitambaza na Viyeyusho.Mfano Konsonanti halisi huwa na sifa ya ukonsonanti pekee na hukosa sifa ya vokali.Kama vile fonimu /p/ .Vokali ni vokali peke yake bila kuwa na sifa ya konsonanti ,kama fonimu /a/, vitambaza ni muunganiko wa konsonanti na vokali, viyeyusho,hivi viko pekee havihusishi konsonanti wala vokali,kama /y/. Uainishaji huu una maana kwamba kuna sauti zinazochangia sifa kama inavyodhihirika katika mfano ufuatao.
 Konsonanti+Vitambaza      [+konsonanti]
 Konsonanti+Viyeyusho       [-Vokali]
 Vokali+Vitambaza              [+Vokali]
 Vokali+Viyeyusho               [-Konsonanti]
Hitimisho.
Kutokana na tofauti za sifa za vitamkwa zilizoelezwa na wataalamu hawa,pia kuna uhusiano wa sifa za vitamkwa kwa kigezo cha uwili.
                                 
   
 MAREJELEO.
Massamba,D.P.(2011).Maendeleo ya Sarufi ya Kiswahili.Nairobi: Phoenix Publishers
Matinde,R.S.(2012).Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia.Mwanza: Serengeti Educational  
        Publishers
Mgullu,R.S.(2010).Mtalaa wa Isimu:Fonetiki,Fonolojia,na Mofolojia ya Kiswahili.Dar-es-
         salaam :Longhorn Publishers.
Hokororo J.I, Kihore Y.M, & Masamba D.P.B, (2003). Sarufi Miundo ya Kiswahili
         Sanifu.SAMIKISA.Dar-es Salaam: TUKI Publisher. 

MKATABA WA KUPANGISHA CHUMBA CHA BIASHARA(FREMU)

  MKATABA WA KUPANGISHA CHUMBA CHA BIASHARA(FREMU)   BAINA YA …………………………………………….. S.L.P ………….., -TANZANIA. Ambaye katika mkataba ...