Imetayarishwa na Mwl.Safari Albert.J,
Simu:+255 715 803 005
barua pepe:salbertode@yahoo.com
Uhakiki ni kazi au kitendo cha kutafakari, kuchambua na kufafanua kazi ya fasihi ili kuweka bayana maadili na ujumbe uliomo katika kazi ya fasihi. Hivyo mhakiki sharti asome kazi ya fasihi andishi au kusikiliza masimulizi kwa makini ili aweze kuyahakiki
Mhakiki ni mtu anayejishughulisha na kazi za kisanaa hususan za kifasihi za wasanii asilia. Mhakiki ni mchambuzi na mfafanuzi wa kazi za kifasihi. Ni jicho la jamii kwani ndiye agunduaye mazuri yaliyomo katika kazi hiyo, hali kadhali mabaya (hatari) yaliyopo katika maandishi hayo kwa jamii husika .
Mhakiki ni bingwa wa kusoma na kuchambua vipengele vya fani na maudhui katika maandishi ya fashihi. Kwa mantiki hiyo mhakiki ni chombo madhubuti cha jamii inayohusika cha kuleta maendeleo katika jamii. Kwa kuzingatia haya anawajibika kuwa mwaminifu, mkweli, asiyeogopa kuweka wazi ubaya uliomo katika maandishi ya mwandishi asilia, na asiyependelea waandishi Fulani Fulani kwa sababu zisizona maslahi kwa jamii. Pamoja na hayo uhakiki wa kazi za fasihi unaambatana na mambo yafuatayo:
(a)Kuisoma kazi ya fasihi kwa makini na kuielewa
(b)Kuchambua vipengele vya fani na maudhui katika kazi hiyo
(c) Kueleza ubora na udhaifu wa matumizi ya vipengele vya fani na maudhui katika kazi hiyo.
Kwa mujibu wa maelezo hayo ni wazikuwa mhakiki anabeba dhima zifuatazo:
1.Kuchambua na kuweka wazi funzolitolewalo na kazi ya fasihi.
2. Kuchambua na kufafanua taswira (picha za kisanii) zilizotumika katika kazi ya mwandishi.
3. Kumshauri na kumtia moyo mwandishi ili afanye kazi bora zaidi (hivyo mhakiki pia ni mwalimu wa mwandishi)
4. Kumwelekeza na kumchochea msomaji kusoma na kupata faida zaidi ya ambayo angeipata pasipo dira ya mhakiki (mhakiki ni mwalimu na daraja kati ya mwandishi na jamii)
5. Kuhimiza na kushirikisha fikra za kihakiki katika kazi za fasihi.
6. Kukuza kiwango cha utunzi na usomaji wa kazi za fasihi.
7. Kutafuta na kuweka sawa nadharia za fasihi teule.
8. Kuthamini na kuheshimu kazi za waandishi kwa kuzitendea haki
VIGEZO VYA UHAKIKI
Kwa kuzingatia kwamba fasihi husawiri jamii katika mfumo mzima wa maisha ya jamiii hiyo mathalani shughuli zinazofanywa katika jamii husika, basi si budi kuzingatia yafuatayo katika kupima kazi ya fasihi:
(i) Ukweli wa mambo yanayoelezwa – mhakiki kama hakimu na daraja atajiuliza, je, ni kweli yaliyoelezwa katika kazi hiyo yanatendeka? Kama anahakiki habari kuhusu ubakaji au rushwa – Anapaswa kujiuliza, Je ni kweli mambo hayo yapo katika jamii ya Tanzania?
(ii) Uhalisia wa watu, mazingira na matukio katika jamii. Hapo mhakiki analinganisha wahusika wa kazi husika na watu halisi ili kuona kama jamii zungumziwa ina watu wanaotenda kama wahusika waliotumika. Mfano habari inaeleza kuwa mganga wa kienyeji aliwapaka dawa watoto wakawaona wachawi, mhakiki anaweza kujiuliza kama kweli hilo linaweza kutokea katika jamiii husika.
(iii) Umuhimu wa kazi hiyo kwa jamii husika lazima uzingatiwe. Jambo linalozungumzwa linaweza kuwa la kweli na linalihalisika lakini lisiwe na umuhimu mkubwa katika jamii kiasi cha kuvuta utayari wa jamii hiyo.
vigezo hivi ndivyo vitumikavyo kupimia vipengele vya maudhui,(dhamira, ujumbe, migogoro, mafunzo na falsafa). Na vipengele vya fani, (muundo, mtindo, matumizi ya lugha, wahusika, na mandhari)
Kwa mfano;
Hadithi inayosifu maisha ya vijijini na kuwashauri vijana wasikimbilie mijini, lazima ipimwe kwa kuzingatia ukweli uliopo vijijini. Mhakiki atajiuliza maswali ya dhamira, mafunzo, migogoro, ujumbe na falsafa kama haya:- Je, ni kweli kuwa wanavijij wana maisha bora kuliko mjini? Je, wanavijiji wanahuduma za lazima kama hospitali zenye waganga na dawa? Je, wanavijiji wana maji salama kwa ajili yao, mifugo na mazao yao? Je, mazao ya wanavijiji yananunuliwa kwa fedha taslimu na mapema? Je, wanavijiji hawa bughudhiwi na wezi, waporaji n.k?
Hali kadhalika mhakikia atajiuliza maswali kadhaa kuhusu kukimbilia mijii, kwa mfano; Je kijana anapokimbilia mjinii ana uhakika wa kupata kazi? Je, kazi kama kuuza machungwa au karanga mijini ni shughuli inayoweza kumkimu huyo kijana? Na Je, vijana wasio na kazi mijini hawalazimiki kuiba au kufanya uhalifu mwingine?
Hatimaye mhakiki atajiuliza maswali kuhusu ufumbuzi unaopendekezwa na mwandishi katika kazi yake, mfano tunaozungumzia mhakiki atajiuliza, je, mwandishi anashauri nini licha ya kusema vijana wabaki vijijini? Je, ni mambo gani anayopendekeza mwandishi kuhusu kuinua shughuli za kiuchumi vijijini? Je., suluhu la mwandishi (mapendekezo) linawezekana (ni yakinifu) au ni la kinjozi tu (la kidhanifu). Msingi wa maswali yote haya ni kujaribu kutambua ukweli, uhalisi na umuhimu wa kauli za mtunzi.
Katika uhakiki wa fani, vipengele vya fani huangaliwa jinsi vilivyotumika na kupima usahihi wake kimatumizi, na hapa maswali huweza kuwa hivi:
-Je, kazi husika ina muundo gani?
-Wahusika wamechorwaje?
-Je, wahusika wanahalisika katika jamii husika?
-Je,mpangilio wa maneno unavutia wahusika?
-Matumizi ya tamathali mbali mbali yanatosheleza haja?
-Misemo na methali zilizotumika zinafaaa hapo zilipotumika au zimepachikwa tu?
VIPENGELE VYA FANI NA MAUDHUI KATIKA KAZI ZA FASIHI ANDISHI:
Riwaya na tamthiliya:
A. Maudhui.
Maudhui katika kazi ya Fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumziwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumlisha mawazo, pamoja na mafunzo mbali mbali yaliyomsukuma msanii hadi kutunga kazi Fulani ya Fasihi.
Vipengele vya maudhui:
1. Dhamira
Hili ni wazo kuu au mawazo mbali mbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi ambayo mwandishi huyajengea hoja. Dhamira hutokana na jamii na zipodhamira kuu na dhamira ndogo ndogo. Dhamira kuu ni zile za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Dhamira kuu ndicho kiini cha kazi ya fasihi na dhamira ndogondogo ni zile zinazoambatana na dhamira kuu.
2. Migogoro
Migogoro ni mivutano na misuguano mbali mbali ambayo huibuliwa na mwandishi katika kazi ya fasihi. Mgogoro kati ya wahusika ama vikundi vya wahusika, familia zao matabaka yao n.k. Migogoro hii mara nyingi hujikita katika mahusiano ya kijamii na ndipo tunapata migogoro ya :
(a) kisiasa
(b) kiuchumi
(c) kiutamaduni
(d) kinafsia (kifikra)
3. Ujumbe na maadili
Ujumbe katika kazi ya fasihi ni mafunzo mbali mbali yapatikanayo baada ya kuisoma kazi ya fasihi. Ujumbe huwa sanjari na maadili mbali mbali ambayo mwandishi amekusudia jamii iyapate.
4. Mtazamo
Ni hali ya kuyaona mambo katika maisha kwa kuzingatia mazingira aliyonayo msanii mwenyewe. Wasanii wana mitizamo ya aina mbili:
(a)Mtazamo wa kiyakinifu – mtazamo huu ni ule wa kuyaangalia mambo waziwazi na kuyaelezea kwa jamii kupitia kazi za kifasihi. Msanii anayeunga mkono mtazamo huu huutazama ulimwengu au mazingira yanayomzunguka binadamu kisayansi na hivyo huelezea mambo katika uhalisia wake.
(b) Mtazamo wa kidhanifu – msanii mwenye mtazamo wa kidhanifu hujadili mambo na kuyatolea masuluhisho yaliyoegemea katika kudhani tu pasipokuzingatia uhalisia wa mambo. Huchukulia ulimwengu kama kitukinachobadilika kulingana na matakwa ya Mungu
5. Falsafa:
Huu ni mwelekeo wa imani ya msanii. Msanii anaweza kuamini kuwa, mwanamke si kiumbe duni kama wengine wanavyoamini au, kwa wale wapinga usawa, wanaweza kuwa na falsafa ya kumwona mwanamke kuwa kiumbe duni au chombo cha starehe.
Hivyo falsafa inatakiwa ichambuliwe kwa kuzingatia jinsi kazi hiyo ilivyoutazama ulimwengu na kuueleza ukweli juu ya mambo mbali mbali na ukweli huo lazima uhusishwe na binadamu.
6. Msimamo:
Hii ni hali ya mwandishi kuamua kushikilia na kutetea jambo Fulani bila kujali kuwa jambo analolishikilia linakubalika au la.
Misimamo ya mwandishi huweza kuwekwa katika makundi (kategoria) matatu:
(a)Msimamo wa kimapinduzi – mwandishi mwenye msimamo huu huyajadili masuala / matatizo yanayoihusus jamii yake na kuonesha bayana – mbinu (njia) za kuondokana na matatizo hayo
(b)Msimamo usio wa kimapinduzi, mwandishi mwenye msimamo huu huwa na asili ya woga inayomfanya kuyajadili mambo kwa kufichaficha na hivyo kushindwa kuleta athari chanya katika mapinduzi.kutokana na kutoonesha bayana masuluhisho ya matatizo aliyoyajadili.
7. Mtazamo
Ni jinsi msanii anavyoyatazama mambo katika ulimwengu wa kifasihi. Hapa tunapata mitazamo ya aina mbili.
(a) Mtazamo wa kiyanifu ambao unaegemea katika kuyajadili mambo kiuhalisia, msanii mwenye mtazamo huu hujadili mambo kama yanavyojitokeza katika jamii. Kwa ujumla mtazamo huu hushadadiwa sana na wanasayansi ambao huhitaji kuthibitisha kila kitu kisayansi.
(b) Mtazamo wa kidhanifu, huu una misingi yake katika kudhani kuwa Mungu ndiye suluhisho la kila kitu hivyo waandishi wenye mtazamo huu hujibainisha wazi kupitia kazi zao hasa kwa kujadili mambo kiujumlajumla mathalani “kuon a kuwa mapenzi bora ndiyo suluhisho la matatizo katika jamii” huu ni mtazamo wa kidhanifu.Wengi wa wanadini hufuata mtazamo huu.
B: Fani
Fani katika fasihi ni ule ufundi wa kisanaa anaoutumia msanii katika kufikisha ujumbe wake kwa jamii inayohusika.
VIPENGELE VYA FANI
1. Muundo
Ni mgawanyo, mpangilio na mtiririko wa kazi hiyo kwa upande wa visa na matukio. Ni jinsi msanii wa kazi ya fasihi alivyoifuma, kuiunda na kuunganisha tukio moja na lingine, sura moja na nyingine, ubeti na ubeti, na hata mstari wa ubeti na mwingine.
AINA ZA MIUNDO:
(a) Muundo wa moja kwa moja/msago
Huu ni muundo wa moja kwa moja ambao matukio huelezwa kwa kuanza la mwanzo hadi la mwisho. Kwa mfano, mhusika huzaliwa, hukua, huchumbia au huchumbiwa, huoa au huolewa, huzaa watoto, huzeeka, hufa. Riwaya ya “Kuli”imetumia muundo huu. Katika riwaya tunamwona Rashidi, akizaliwa, akiwa, anaanza kazi, anaoa, anaanza harakati za kudai haki za makuli namwisho anafungwa.
(b) Muundo wa kioo/rejea
Huu ni muundo unaotumia mbinu rejeshi ambayo huweza ama kumrudisha nyuma msomaji wa kazi ya fasihi katika mpangilio wa matukio yake au kuipeleka mbele hadhira ya kazi hiyo. Riwaya ya “Zaka la Damu” imeutmia muundo huu.
(c) Muundo wa rukia
Huu ni muundo ambao visa na matukio hurukiana. Katika muundo huu kunakuwa na visa viwili ambavyo hurukiana katika kusimuliwa kwake, na mwisho visa hivi huungana na kujenga kisa kimoja. Mfano Njama.
2. Mtindo:
Mtindo katika kazi ya fasihi ni ile namna ambayo msanii huiwasilisha kazi yake kwa jamii. Ni upangaji wa fani na maudhui katika kazi ya fasihi kwa njia ambayo hudokeza upekee wa mwandishi.
Dhima ya mtindo
· Humwezesha msomaji kujua hisia za mwandishi juu ya aliloliandika.
· Hudokeza kiasi cha hisia na mwamko wa wahusika katika hadithi.
· Kuonesha mtiririko (muwala) wa matukio.
· Kuumba ulimwengu ambao utabeba maono ya msanii. Lengo ni kuepusha mifarakano inayoweza kujitokeza. Kwa mfano, katika riwaya ya “Kusadikika” ambayo imeumbiwa ulimwengu ulioko angani na nchi inayoelea.
Katika mtindo huangaliwa:
-Matumizi ya lugha
-Nafsi zilizotumiwa
-Matumizi ya monolojia (maelezo/ masimulizi) na dialojia (majibizano).
-Mbinu ya kutumia tanzu nyingine za fasihi simulizi
-Matumizi ya hadithi ndani ya hadithi
-Matumizi ya barua n.k.
Jambo la msingi katika mtindo ni lugha, na ndiyo inayotofautisha fasihi na sanaa nyingine kama vile uchoraji, uchongaji, usukaji, ufinyazi n.k. Msanii wa fasihi chombo chake (nyenzo) ni lugha.
3. Wahusika:
Wahusika ni watu, vitu ama viumbe waliokusudiwa kubeba dhamira mbalimbali kwa lengo la kuwakilisha tabia za watu katika kazi ya fasihi.
Aina za Wahusika:
(a) Wahusika Wakuu:
Hawa ni wale ambao wanajitokeza kila mara katika kazi za fasihi, hutokea tangu mwanzo hadi mwisho. Wahusika hawa hubeba kiini cha dhamira kuu na maana ya hadihti yote. Vituko, visa na matendo yote hujengwa kuwahusu au kutokana nao. Mara nyingi jambo hili limewafanya wahusika wakuu wa kazi ya fasihi wawe “midomo” ya wasanii, na pia vipaza sauti vya watunzi wa kazi za fasihi. Wahusika wakuu hasa wameelezwa kwa mapana na marefu juu ya maisha na tabia zao ili kuukamilisha unafsi wao.
(b) Wahusika wadogo / wasaidizi
Hawa hujitokeza hapa na pale katika kazi ya fasihi ili kuukamilisha ulimwengu wa kazi hiyo. Hawa husaidia kuijenga dhamira fulani katika kazi ya fasihi na hasa hubeba dhamira ndogo na kwa minajili hiyo huitwa wahusika wadogo ingawa wakati Fulani husaidia kujenga na kuikamilisha dhamira kuu.
(c) Wahusika wajenzi:
Hawa ni wahusika ambao wamewekwa ili kukamilisha dhamira na maudhui Fulani, kuwajenga na kuwakamilisha wahusika wakuu na wasaidizi. Wahusika wakuu na wadogo huweza kuwekwa katika aina tatu:
(i) Wahusika Bapa;
Hawa ni wahusika ambao hawwabadiliki kitabia wala kimawazo kulingana na mazingira au matukio ya wakati wanayokutana nayo. Wahusika bapa huweza kugawanywa kwenye makundi mawili:
Wahusika Bapa – sugu-
Hawa huwa sugu katika hali zote, kiasi kwamba hata tuwaonapo mahali pengine hali zao ni zile zile, wao ndio huhukumu hushauri na kuongoza tu na si vinginevyo wanakuwa kama madikteta. Mfano” Bwana Msa” katika riwaya ya “Mzimu wa watu wa kale” ya M.s. Abdulla.
Wahusika bapa – vielelezo –
Hawa pamoja na kutobadilika kwao, hupewa majina aghalabu ya kiishara ambayo – humfanya msomaji aelewe tabia na matendo yao. Mfano: “Waziri Majivuno”, “Adili”, Utubora” na “Karama” katika kazi za “Shaaban Robert” ni mfano wa wahusika bapa wala, kiasi ambacho anaondoa sehemu zote za sifa za wahusika huyo.
(ii) Wahusika duara / mviringo
Hawa ni wahusika ambao hubadilika kitabia, kimawazo ama kisaikolojia. Maisha yao hutawaliwa na hali halisi yamaisha. Hivyo wanavutia zaidi kisanii, kwani husogeza hadithi ielekee kwenye hali ya kutendeka au kukubalika na jamii.Mfano, (Rose mistika) , Josina (pepo ya mabwege)
(iii) Wahusika shida / foili
Hawa ni wahusika ambao huandamwa na shida, misukosuko na taabu na wahusika hawa hutokea kati ya wahusika bapa na duara. Wahusika shida huwategemea wahusika duara au bapa ili waweze kujengeka. Mfano: “Najum” katika riwaya y’’ Mzimu wa Watu wa Kale’’ na m.s Abdulla.
4. Matumizi ya lugha
Lugha ndiyo njia (nyenzo) aitumiayo msanii wa fasihi kuyaelezea mambo mbali mbali yahusuyo jamii kwa njia ya ubunifu na usanii. Hivyo lugha ndiyo mzizi wa kazi ya fasihi na bila yenyewe kuwapo haiwezekani kuwa na fasihi.
Vipengele vya lugha
(i) Methali
Methali ni tungo fupi zenye hekima na busara ndani yake ambazo hutumika kama kiungo cha lugha kwa lengo la kufunzia na kupenyeza hekima kwa jamii kupitia fashi.
Methali pia hutumika kujenga mandhari ya kiutamaduni ya kuaminika kuhusu jamii itumiayo methali hizo. Hivyo huweza kusemakuwa pale ambapo methali zimetumika katika kazi mbali mbali za fasihi, nyingi zimejenga fani na maudhui ya kazi hizo.
(ii) Misemo na nahau
Matumizi ya misemo na nahau katika kazi za fasihi hushabihiana sana na yale ya methali. Misemo na nahau hutumika kwa madhumuni anuai kama vile kutambulisha mazingira, na wakati husika wa kazi hiyo, lakini pia kupamba kazi ya fasihi pamoja na kuitajirisha lugha ya msanii katika Kazi yake.
(iii) Tamathali za semi
Tamathali za usemi ni maneno ambayo hutumiwa na wasanii wa fasihi ili kutia msisitizo, nguvu na maana katika kazi zao, hali kadhalika kuboresha mtindo wa kazi zao. Wakati mwingine huwa na lengo la kupamba kazi ya fasihi na kuongeza utamu wa lugha. Kuna aina nyingi zatamathali za usemi kama ifuatavyo;
(a)Tamathali za mafumbo
Dhihaka (sarcasm)
Hii ni tamathali ya dharura na ina lengo la kumweka mtu katika hali duni kupita kiasi, lakini kwa mbinu ya mafumbo
Mfano:
“Adella alikuwa msichana msafi sana. Ndiyo maana kila, mara alipata kupaka mafuta yaliyonukia na kukaribisha nzi walioleta matatizo makubwa”.
Tafsida (Euphemism)
Hii hupunguza ukali wa maneno au utusi katika usemi
Mfano:
-Kujisaidia au kwenda haja badala ya kunya au kukojoa.
-Kuaga dunia badala ya kufa n.k
Kejeli / shitizai (Irony)
Hii imekusudiwa kuleta maana iliyo kinyume na ile iliyokusudiwa ama kinyume na ukweli ulivyo. Lengo lake ni kutaka kuzuia matatizo na migongano pindi itumikapo kwa lengo maalumu la kufundisha na kuasa.
Mfano:
-Mtu ni mchafu, lakini anaambiwa –sijamwona mtu msafi kama wewe.
-Mtu ni adui, lakini anambiwa – wewe ni rafiki mpenzi
-Mtu ni mweusi kama mkaa – anaitwa cheupe.
Kijembe / kiringo (Innuendo)
Huu ni usemi wa mzunguko, ni usemi wa kimafumbo wa kumsema mtu kwa ubaya.
(b)Tamathali za mliganisho
Sitiari (Metaphor)
Ni tamathali inayolinganisha matendo, vitu au tabia ya vitu vyenye maumbile tofauti bila kutumia viunganishi linganishi
Mfano:
-Maisha ni moshi
-Pesa ni maua
-Penzi upepo
-Misitu ni uhai
Tashibiha (simile)
Tamathali inayolinganisha vitu kwa kutumia maneno kama vile mfano wa, kama, mithili ya , sawa na , n.K
Mfano
-Ana sauti tamu sawa na ya chiriku
-Ana maringo kama twiga
-Ananyata mithili ya kinyonga
-Ana ng’ang’ania kama kupe.
Tashihisi (personification)
Tamathali hii huvipa vitu sifa walizonazo binadamu (hupewa uwezo walionao binadamu)
Mfano:
-Mvua iliponyesha misitu ilipiga makofi
-Mawimbi yalitabasamu kwa upepo wa kusi.
Lakabu
Katika tamathali hii uhusiano wa maneno mawili kisarufi hugeuzwa na pengine huwekwa kinyume na taratibu za kisarufi zilivyo
Mfano:
-Baridi kali ilimkaribisha (lakini mtu ndiye mwenye uwezo wa kukaribisha)
-Giza liliwapokea walipokuwa wakiingia pangoni
(c)Tamathali za msisitizo na nyinginezo
Mubaalagha (Hyperbole)
Hii hutia chumvi kuhusu uwezo wa viumbe, tabia zao na hata sifa zao kwa madhumuni ya kuchekesha au kusisitiza
Mfano:
-Loo! Hebu muangalie mrembo yule! Ana mlima wa kiuno
-Tulimlilia Nyerere hadi kukawa na bahari ya machozi
-Mrembo yule hubeba kila aina ya silaha na huwatia wazimu wanaume wote anaokutana nao.
Taashira / metonumia (metonymy)
Katika tamathali hii jina la sehemu ya kitu kimoja au la kitu kidogo kinachohusiana na kingine kikubwa hutumiwa kuwakilisha kitu kamili.
Mfano:
-Jembe huwakilisha mkulima
-Kutabasamu huwakilisha furaha
-Mvi huwakilisha uzee
-Kalamu huwakilisha mwanafunzi / msomi.
Majazi
Hii ni aina ya sitiari ambayo itajapo sehemu tu ya kitu hapo hapo sehemu hiyo huashiria na kuwakilisha kitu hicho.
Mfano:
Roho – mtu
-Masikini, ajali ile ilipoteza roho tano hapo hapo]
Taniaba (Antonomasia)
Hii ni tamathali ambayo kwayo jina la mtu binafsi hutumiwa kwa watu wengine wenye tabia, mwenendo, hali au kazi sawa na ya mtu huyo.
Mfano:
-Yesu – mkombozi
-Yesu wa kwanza wa Afrika alikuwa Kwame Nkrumah
-Nyerere alikuwa Yesu wa kwanza Tanzania
Tabaini (antithesis)
Hii ni usemi unaosisitiza jambo kwa kutumia maneno ya ukinzani (unyume)
Mfano:
-Mwanadamu hupanga Mungu hupanga
-Amekuwa mrefu si mrefu, mfupi si mfupi ni wa kadiri
-Usimwamini mtu, yu acheka machoni, rohoni ana mabaya.
(d)Mbinu nyingine za kisanaa
Takriri (Tautology)
Hapa yanakuwepo marudio kwenye sentensi au kwenye usemi na lengo ni kusisitiza
Mfano:
-Dunia ni ngumu jamani, ni ngumu
-Haba na hapa hujaza kibaba
Mdokezo (Aposiopesis)
Hapa msemaji au mwandishi hukatiza maneno au huacha maneno bila kutaja kitu au maneno ambayo kwa kawaida ni wazi na huweza kujazwa kwa ubunifu.
Mfano:
-Ally alipokuwa analia alisema………………
-Watu wengi huambukizwa ukimwi kwa kushiriki ………………
Tashtiti (Rhetorical Questions)
Ni mbinu ya kuuliza maswali kwa jambo ambalo majibu yake yanafahamika.
Mfano:
-Asha na uzuri wake amekufa?
-Loo! Asha ametutoka?
-Hatakuwa nasi tena?
Nidaa (!)
Huu ni msemo unaoonesha kushangazwa na jambo Fulani. Msemo huu huambatana na alama ya kushangaa
Mfano:
-Baba ndiye amefariki!
-Ah! Havijawa nimekutoroka!
-Hakika nitakupenda!
Mjalizo (Asyndeton)
Hapa huwa ni mfuatano tu wa maneno yasiyo na viunganishi vyovyote bali hutengwa kwa alama ya mkato(,)
Mfano:
-Nilikaa, nikasubiri, nikachoka
-Nilipanda, nikapalilia, nikavuna, nikauza, nikajenga nyumba.
Tanakali sauti (onomatopeia)
Ni mbinu ya kuiga sauti za milio mbali mbali. Milio hii ni ya wanyama, magari, vitu n.k
Mfano:
-Alitumbukia majini chubwi!
-Alidondoka chini pu!
(e) Taswira
Ni picha zinazojitokeza ndani ya mawazo ya msomaji au msikilizaji wa kazi ya fasihi. Matumizi mazuri ya taswira na ishara hutegemea ufundi wa yanayomzunguka yeye na jamii yake pamoja na historia za maisha azijuazo.
Aina za Taswira
(i)Taswira za hisi
Taswira hupenyeza hisia na kuzigandisha akilini mwa msomaji au msikilizaji na kunasisha ujumbe wa mwandishi. Taswira hizi hushughulikia hisi za ndani, na kuweza kumfanya msomaji au msikilizaji awe na wasi wasi aone woga, apandwe na hasira, ahisi kinyaa, n.k
mfano:
Akadharau! Siwezi kula chakula kama hicho! Rojorojo nyororo kama limbwata, mfano wa kohozi lenye pumu,liingie katika koo langu lililozoea kuku wa mrija
-Maelezo hayo humfanya mtu akinahi na kutaka kutapika mara akisoma rojorojo, kunyororoka mfano wa kohozi lenye pumu.
(ii)taswira za mawazo / kufikirika
Hizi zinatokana na mawazo yahusuyo mambo yasiyoweza kuthibitika. Mambo kama kifo, pendo, uchungu, fahamu, sahau, raha n.k
Mfano:
Kifo umefanya nini? Umeninyang’anya penzi langu bila huruma? kumbuka, nilimpenda nikapoteza fahamu, kifo ukazidi kunidunga sindano ya makiwa?
(iii) Taswira zionekanazo
Hizi ni picha ambazo hujengwa kwa kutumia vielelezo tunavyovijua vile vinavyofahamika katika maisha ya kila siku.
Mfano:
Dakika haikupita mijusi wawili wliokuwa wamebebana walipita haraka. Midomo yao ilikuwa myekundu. Ghafla walikutana nanyoka aliyeonekana mnene tumboni. Hapana shaka alikuwa amemeza mnyama.
5.Mandhari / mazingira
Ni sehemu ambamo kazi ya fasihi inafanyika. Mandhari yaweza kuwa ya kubuni kama” Kusadikika” na “Kufikirika” au halisi (ya kweli) mfano mandhari ya Dar es salaam, Arusha n.k. kwa Tanzania.
6 Jina lakitabu / Jalada la kitabu
Hapo tunaoanisha jina la kitabu na yaliyoelezwa ndani ya kitabu hicho. Mfano”Kiu ya Haki”, jina hili linasadifu vipi yaliyomo ndani ya riwaya hiyo. Je, kweli yaliyoelezewa yanadhihirisha kiu ya haki? Pia tunaangalia picha mbali mbali zilizochorwa juu ya jalada la kitabu na kutafsiri kifasihi jinsi picha hizo zilivyotumika.
7.Kufaulu na kutofaulu kwa mwandishi kifani na kimaudhui
Hapa tunaangalia ubora na udhaifu wa mwandishi kifani na kimaudhui katika kazi husika. Hapa vipengele vya fani na maudhui huzingatiwa kwa kina ili kuweza kupima umadhubuti wa kazi hiyo na hatimaye kuamua kwa haki kama mwandishi amefaulu au hajafaulu.