Saturday, 3 March 2018

MAMBO 5 YA KUZINGATIA KATIKA MAISHA

Utangulizi

Maisha ni muda ambao kiumbe hai anajaliwa kuishi. Ni hali tofauti kabisa na uzima wa milele , kwa kuwa uhai wake una mwanzo na mwisho.
Hasa mwisho unasababisha maswali: kama kila chenye mwanzo kina mwisho, ya nini kuwepo kwake? Kukosa lengo, kuwepo bure, kutokuwa na maana kunamfanya mtu ajisikie mnyonge, pengine akate tamaa ya kuishi, la sivyo ajitose kufurahia mazuri yanayopatikana maishani, lakini bila uwezo wa kuondoa moyoni ule utupu wa maana unaomtia huzuni ya dhati.
Ndiyo sababu maana ya maisha ni mojawapo kati ya masuala makuu ya binadamu duniani: hawezi kukwepa maswali ya kutoka moyoni mwake kuhusu thamani, madhumuni na umuhimu wa maisha yake.

Mambo 5 ya kuzingatia katika maisha:

1.HOFU YA MUNGU;
Hofu ya Mungu : Hii ni ile nguvu ya Mungu ndani ya mtu inayomfanya asitende dhambi (MWANZO 20:11), Neno hilo linatuonesha kisa cha Ibrahimu baada ya kuona kwamba Wagerari hawana hofu ya Mungu ndani yao na watamuua wakijua Sara ni mkewe kwa alivyokua mzuri, aliamua kuwaambia kwamba ni Dada yake. Ibrahimu aliamua kufanya hivyo kulinda uhai wake. Simaanishi kwamba alikuwa sahihi kusema uongo, lakini nilitaka tuone kwamba hofu ya Mungu ikoje.
Ni ukweli usiopingika kwamba, hakuna mwanadamu anayeweza kuishi maisha matakatifu kama hakuna hofu ya Mungu ndani yake ; hofu ya Mungu huletwa na uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu. Ukiona wewe bado unafanya dhambi na huoni moyo wako ukikuhukumu, basi we jua bado unamwitaji Mungu sana. Ingawa wako ambao wakitaka kufanya dhambi wanahisi kuhukumiwa ndani yao ila wanajikaza kutenda dhambi kwa lazima. Ukiona uko hivyo, bado hofu ya Mungu haimo ndani yako.
Mara nyingi mwanadamu anapotaka kufanya dhambi, huwa anatafuta sehemu iliyojificha ili kwamba Mchungaji wake, wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wasiweze kumwona.

2.MUDA;
Muda ni kipindi ambacho mtu aidha alifanya, anafanya au anatarajia kufanya jambo fulani. Katika maisha ya kila siku mwanadamu hutegemea sana muda ili kufanikisha malengo yake.

3.MAAMUZI;
Kwanza kabisa maamuzi ni neno kubwa sana na lenye maana nzito kuliko tunayoitumia kila siku. Unaposema umefanya maamuzi maana yake ni umeondoa uwezekano mwingine wowote wa wewe kufanya jambo tofauti na ulilolifanyia maamuzi. Maana halisi ya maamuzi ni kwamba umechagua kitu kiwe hivyo tu, au umeamua kufanya kitu ulichokiwekea maamuzi na sio kitu kingine hasa kinachopingana na hicho.
Lakini katika maisha yetu ya kila siku tunafanya maamuzi na muda mfupi baadae unavunja maamuzi uliyofanya mwenyewe.
Unasema kuanzia sasa nitajisomea na kujifunza kila siku ili kuweza kupata maarifa yatakayoniwezesha kufikia mafanikio makubwa zaidi. Lakini baada ya muda unaanza kuona kujifunza ni jambo la kawaida na kutokufanya tena kila siku. Hapa ndio unaanza kurudi nyuma, na usiposhtuka mapema utapotea vibaya mno.
Kati ya vitu ambavyo ni lazima ufanyie maamuzi katika maisha yako ni kuamua kuwa hautakubali kushindwa katika maisha yako.

4.MARAFIKI;
Marafiki zako wana nguvu ya kukufanya ufanikiwe ama kukufanya ushindwe kufanikiwa.Kuna watu wengi sana ambao wameshindwa kabisa kufikia katika kilele cha hatima zao kwa sababu tu wameendekeza kuwa na marafiki ambao wamekuwa kikwazo kwa maisha yao.Ila kuna wengine wameshindwa kabisa kufikia kilele cha mafanikio yao kwa kushindwa kutumia vizuri marafiki walionao.Siku zote kumbuka kuwa kila rafiki uliye naye lazima anakuathiri kwa namna fulani-Inawezekana akakuathiri kwa uzuri(Positive) ama akakuathiri kwa ubaya(Negative).Kwa sababu hii,ni lazima kila wakati uwe mtu ambaye unatathmini kuhusu maisha yako na wale wanaokuzunguka na jinsi wanavyochangia kukufanikisha ama kukukwamisha.

5.MALENGO;
Kuwa na malengo ni moja ya chachu kubwa ya mafanikio katika jambo lolote unalofanya kwenye maisha. Malengo yanakupa dira maishani mwako na kukuelekeza usiende mrama kwa kukosa mwelekeo. Malengo yanaweza kuwa vitu vidogo tunavyotaka kubadili leo, pia yanaweza kuwa mambo makubwa tunayotaka kuyafanikisha siku zijazo, iwe baada ya mwezi, mwaka, au hata baada ya miaka mitano! Unaweza ukawa na malengo ya aina mbalimbali; ya kiafya, kikazi, kimasomo, kiuhusiano au kibiashara; jambo la muhimu ni wewe kuwa na malengo.
“Funga macho, vuta picha ya magari mawili yanatembea. Dereva mmoja anajua kuwa anatoka kijiji A na kwenda kijiji B, halafu dereva wa pili wala hajui anakokwenda. Kati ya madereva hao wawili, yupi atafika anakokwenda? Bila shaka jibu litakuwa ni dereva A. Kinachowatofautisha ni malengo, dereva wa gari la kwanza anajua kuwa lengo lake ni kufika kijiji B, hapo atatafuta hata njia ya mkato afike, hata kama hajui njia anaweza akauliza watu akaelekezwa. Dereva wa pili hata kama kuna barabara mbele yake anaweza akafika anakotakiwa kwenda, akapapita au akageuza maana hajui anakokwenda”.

HITIMISHO:
Katika maisha ya mwanadamu kuna mambo mengi tunakutana nayo na mengine ni matokeo ya maisha tunayoishi leo hii.
Kuna mambo kama elimu,umri,mapato,matumizi,mahusiano,tabia na n.k yote haya yana athari chanya na hasi katika maisha ya mwanadamu.Ingawa ukiangalia kwa undani utabaini kuwa mambo tuliyotaja yanagusa nyanja zote hizo na kama yakizingatiwa yatamuwezesha binadamu kuyatawala maisha yake.

No comments:

Post a Comment

MKATABA WA KUPANGISHA CHUMBA CHA BIASHARA(FREMU)

  MKATABA WA KUPANGISHA CHUMBA CHA BIASHARA(FREMU)   BAINA YA …………………………………………….. S.L.P ………….., -TANZANIA. Ambaye katika mkataba ...