KUKUA NA KUENEA KWA LUGHA YA KISWAHILI
Barua Pepe:salbertode@yahoo.com
Namba ya simu: +255 715 803 005
Kuna mambo
mbalimbali yanayofanya lugha yoyote ikue. Mambo hayo ni kama vile matumizi ya
lugha katika shughuli mbalimbali kama vile:
·
Shughuli za utawala na kampeni za kisiasa.
·
Shughuli za kibiashara ndani na nje ya nchi.
·
Maswala ya Elimu.
·
Mikutano ya nchi (kitaifa) na kimataifa.
·
Shughuli mbalimbali za kiutamaduni, muziki, sherehe, nk.
·
Matumizi
ya lugha katika vyombo vya habari kama vile magazeti, redio, televisheni, nk.
·
Urahisi
wa lugha yenyewe katika kueleweka na kuweza kuchukua maneno ya kigeni au maneno
ya utamaduni wa mataifa mengine bila mgogoro.
Urahisi huo wa lugha
waweza kuwa katika:
(i) Matamshi yake
(ii) Msamiati
(iv) Miundo
(v) Maana-:mfano neno moja kuwa na maana
zaidi ya moja, nk.
(vi) Mwingiliano wa tamaduni mbalimbali na
uhamiaji wa kigeni.
(vii) Vita-husababisha
kuchangamana kwa watu wengi pamoja na hivyo huweza kusababisha lugha ya
utamaduni fulani kuenea na kukua haraka ukilinganisha na lugha za tamaduni
nyingine.
(viii) Usanifishaji-husababisha
lugha fulani iteuliwe kutumika katika nyanja fulani kama elimu, utawala, biashara,
nk. Na hivyo lugha hiyo hukua. Kutokana na usanifishaji ndipo tunapata lugha
rasmi na lugha ya taifa.
Hivyo kukua kwa lugha ni hali ya kuongezeka kwa
msamiati. Msamiati ni jumla ya maneno yanayotumiwa katika lugha fulani. Ili
lugha yoyote ikue lazima msamiati wake ukuzwe.
Sababu za uundaji wa
msamiati/maneno ni kama zifuatazo:
(a) Kwa
ajili ya matumizi ya kawaida ambayo huchukua
sura
mpya kila siku.
(b) Kwa
ajili ya kuweza kutafsiri mengi kutoka lugha yako kwenda lugha ya kigeni au
kutoka lugha ya kigeni kuingia katika lugha yako.
(c) Ili
kupata msamiati unaokubalika na shughuli mahsusi kama vile benki, forodhani,
Jeshini, nk.
(d) Kwa
ajili ya matumizi ya utamaduni wa watu wa taifa hili
au
hata taifa jingine. Jambo la muhimu ni kuona msamiati wa Kiswahili unaendelezwa
ili kukidhi haja ya watumiaji wa Kiswahili katika kupokea maingiliano ya fani
mpya za utamaduni wa kigeni.
(e) Ili
kukidhi msamiati wa masomo yote katika lugha yako, ambayo hapa ni Kiswahili.
KUENEA KWA KISWAHILI NCHINI TANZANIA
Lugha kusikika imeenea kama kuna ongezeko la watu wanaoitumia lugha
yenyewe ndani ya nchi husika. Ongezeko hilo linakomaa kiasi cha kuvuka mipaka
ya awali. Leo hii, Kiswahili kinazungumzwa si nchini Tanzania tu, bali pia nje
ya mipaka yake: Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo, Zambia, Malawi na Msumbiji.
1 Kabla ya
Ukoloni
Kuenea kwa Kiswahili
nchini Tanzania kabla ya ukoloni kulikuwa wakati wa biashara ya waafrika
wenyewe kwa wenyewe. Biashara hii, ilikuwa imeshamiri sana, si nchini Tanzania
tu, bali pia katika upwa wote wa Afrika Mashariki.
Wenyeji wa pwani na
wenyeji wa bara, hususan Tanzania, walikuwa na mawasiliano ya muda mrefu kabla
ya kufika wageni wa Kiarabu na Kizungu. Kulikuwa na safari za kibiashara baina
ya Pwani na Bara zilizokuwa zikifanywa na Waafrika wenyewe. Katika safari hizo,
watu wa Bara walikitumia Kiswahili cha pwani na kukieneza sehemu za Bara, sio
tu wakati waliporejea makwao kuwataka hali ndugu na majirani zao waliowaacha
kwa miaka kadhaa, bali pia wafanyabiashara hao walipokuwa wakifanya biashara
zao na Waarabu. Kwa mantiki hiyo, ndio walioanza, bila kukusudia, kuieneza
lugha ya Kiswahili kutoka Pwani hadi sehemu za Bara za Tanzania.
Wageni
waliohusika walioshirikiana na Wenyeji katika kueneza Kiswahili nchini Tanzania
wakati wa ukoloni walikuwa Waarabu, Waajemi, Wareno, Wajerumani na Waingereza.
Sababu zilizowafanya waje Afrika Mashariki, husasani Tanzania, ni pamoja na
kufanya biashara, kueneza dini na kutawala.
3
Kutokana na Biashara
(i) Waarabu
Kwa mujibu wa
maelezo ya Nkwera (2003:119) Waarabu walifika Pwani ya Afrika Mashariki karne
ya kumi. Walipofika hapa waliwakuta wenyeji wanazungumza Kiswahili, na kutokana
na nia ya kueneza biashara yao, Waarabu wanajulikana sana kwa biashara, hususan
biashara ya watumwa. Walishirikiana sana na watumwa katika dini, biashara na
kuoana.Waarabu hao waliitumia lugha ya Kiswahili kila walipopita kufanya
biashara yao. Lugha ilikuwa muhimu sana kwa mawasiliano kwa kila jambo
walilofanya kati yao na wenyeji wao, hususan kwa kuwatumia watumwa wao.
Kwa kufanya hivyo,
walijikuta wameeneza lugha ya Kiswahili.
Katika kuhakikisha
kuwa lugha hii inafundishwa vyema na biashara inaendelea bila tatizo, Waarabu
walianzisha vituo maalum kwa ajili ya biashara na wakati huo huo kufundisha
dini ya Kiislamu. Vituo vya kibiashara kama vile Tabora na Ujiji vilikuwa na
umuhimu mkubwa sana katika kueneza dini ya Kiislamu na Kiswahili hapa nchini.
(ii) Wajerumani
Wajerumani walianzisha mashamba makubwa ya mazao ya biashara na
wakalazimisha Watanganyika kutoka Bara na Pwani kufanya kazi ya kulima katika
mashamba hayo, hususan mashamba ya
Mkonge (katani). Kwa kuwa walikuwa
watu wa makabila mbalimbali, Kiswahili kilitumika sana katika mawasiliano baina
yao. Na wale waliobahatika kurejea nyumbani, walisaidia kukieneza Kiswahili
huko kwao.
4 Kutokana
na Dini
(i) Waarabu na Dini ya Ki-Islamu
Walipofika karne ya 10 waliwakuta wenyeji wakizungumza lugha zao za
Kibantu kikiwemo Kiswahili. Waarabu walipofika na dini ya Kiislamu
walijikuta wakishirikiana na wenyeji wa upwa huu
katika mambo makuu matatu; Dini, biashara na kuoana.
Ili waweze kueneza dini yao vyema, Waarabu walijifunza kwa dhati lugha
ya Kiswahili. Kwa vile walijishughulisha pia na biashara, Waarabu waliweza
kujumuisha mambo mengi kwa mara moja.
(ii)
Wamishenari na Dini ya Ki-Kristo
Hawa
walifika pwani ya Afrika Mashariki kabla ya utawala wa Wakoloni. Mashirika
mbalimbali ya kidini yaliingia Afrika Mashariki katika nyakati tofauti tofauti.
Mashirika haya ni “Roho Mtakatifu” toka
Ufaransa mwaka 1868, White Fathers
toka Ufaransa mwaka 1878, Church
Missionary Society (CMS) ambalo liliongozwa na J.C. Krapf kutoka Ujerumani.
Shirika hili mwaka 1876 liliandika sarufi ya kwanza ya Kiswahili cha Kimvita
katika kitabu kilichoitwa Outlines of the
Elements of Kiswahili Language with Specific Reference to the Kinika Dialect.
Pia
mwaka 1845, Krapf alimpelekea katibu wa CMS orodha pana ya maneno (muhtasari)
wa sarufi pamoja na tafsiri ya Injili ya Luka na Yohana ili kuwasaidia
Wamishenari wengine ambao walikuwa wakiletwa Afrika ya Mashariki. Mwaka 1905
Misioni ya Magila walitoa kijitabu juu ya historia ya Wasambaa kilichoitwa Habari za Wakilindi. Makao makuu ya
shirika hili yalikuwa Mombasa.
Shirika
la Universities Mision to Central Afrika
(U.M.C.A) (Uingereza) liliingia mwaka 1875 nchini, UMCA
ilijishughulisha sana na kukiweka Kiunguja katika maandishi waka 1870 Askofu
Edward Steere alichapisha toleo la kwanza la sarufi ya Kiswahili cha Kiunguja
lililoitwa “A Handbook of the Swahili
Language as Spoken at Zanzibar”. Pia walichapisha vitabu vya nyimbo na
kamusi za Kiswahili na Kiingereza-Kiswahili kazi ya awali ya kuziandaa kamusi
hizo ni ya Edward Steere, lakini ilikamilishwa na A. Madan na baadaye kurudiwa
na F. Johnson aliyeandaa kamusi mbili A
Standard English-Swahili Dictionary na Swahili
English Dictionary ambazo zilitolewa mwaka 1939. UMCA walichapisha pia
magazeti ya Msimulizi (1888), Habari za Mwezi (1876), Pwani na Bara (1910).
Kwa ujumla wamisheni walijishughulisha sana na
Kiswahili kwa sababu walikihitaji katika shughuli zao za kidini kwa kufanya
hivyo walijikuta wanaikuza na kuieneza lugha ya Kiswahili kwa kiasi kikubwa
kufuatana na uongezekaji wa vituo vyao nchini. Baadhi ya vituo hivyo ni
Bagamoyo (1868), Magila (1864), Mpwapwa (1876), Ujiji (1877), Masasi (1876),
Zanzibar (1860) na Ziwa Nyasa (1881).
5 Kutokana
na Utawala
(i) Kutokana na Utawala wa Wajerumani
Tunafahamishwa na
Nkwera (2003:120) kwamba Wajerumani wameitawala Tanganyika kwa miaka thelethini
(30) yaani (1885 – 1916) kwa jina
la Deutsch Ost Afrika (Afrika ya Mashariki ya Mjerumani).
Wajerumani walipoingia Tanganyika walikuta tayari kuna misingi mizuri
ya lugha ya Kiswahili, Wamisheni walikuwa tayari wameandaa mfumo wa elimu na
dini uliokuwa unatumia lugha ya Kiswahili. Kutokana na misingi hiyo utawala wa
Kijerumani ulipoanzishwa nchini Kiswahili tayari kilikuwa kimeimarika.
Kwa hiyo, Wajerumani walikiona Kiswahili kuwa ni chombo muhimu sana kwa
kuwasiliana na wananchi katika mawanda yafuatayo:
(a) Kiswahili kilitumiwa na wamisionari
kueneza Injili.
(b) Katika
Shule za watoto wadogo (Chekechea), Shule za Misingi na Shule za Kati (Middle
Schools), Wamisionari walitumia Kiswahili kufundishia kuandika, kusoma,
kuhesabu na kazi mbali mbali za ufundi, k.v. useremala, uashi na ufyatuaji
mataofali.
(c) Kwa
upande wa Seriali, Kiswahili kilitumika kuelezea na kuenezea siasa ya
Kijerumani na mipango ya Serikali kwa wananchi, na pia kuendeshea shughuli za utawala.
Kwa mantiki hii, Wajerumani walisisitiza sana kwamba
Kiswahili kifundishwe mashuleni kote, na Kijerumani kifundishwe katika madarasa
ya Elimu ya Watu Wazima. Walilazimisha
kila Akida afahamu Kiswahili barabara ili aweze kutumwa na kufanya kazi mahali
popote, siyo tu katika sehemu aliyozaliwa na kukulia.
(e) Wajerumani walijenga shule Tabora, Ujiji,
Kilimatinde, Kasangu mwaka 1905 na hatimaye Bukoba, Mpwapwa, Iringa, Mwanza,
Kilosa, Tukuyu na Moshi. Vyuo vya kufundishia Walimu vilianzishwa huko Tabora
na Bukoba.
Kutokana na Wajerumani kusisitiza
matumizi ya Kiswahili katika shughuli za utawala, shule, kortini (mahakama) na hata katika kuwasiliana
na wananchi, walisaidia sana kukieneza Kiswahili sehemu mbalimbali za
Tanganyika.
(ii) Kutokana
na Utawala wa Waingereza
Baada
ya ujio wa Waingereza Tanganyika, juhudi mbalimbali zilifanywa katika kueneza
Kiswahili nchini. Kwanza ilikuwa ni kuteua aina moja tu ya Kiswahili ambayo
ingetumika katika nchi zote nne za Afrika Mashariki. Pia uwepo mtindo mmoja wa
kukiandika. Hivyo mwaka 1928 mkutano ulifanyika Mombasa na walikubaliana kuwa
nchi zote nne zitumie lugha ya aina moja yaani Kiunguja.
Mwaka
1929 Katibu wa halimashauri ya magavana wa Afrika Mashariki aliziandikia
serikali nne kuhusu suala la kuanzishwa kamati ya lugha ya serikali zote nne na
tarehe 1-1-1930 kukaanzishwa kamati iliyoitwa Inter-Territorial Language (Swahili) Committee ili ihusike na
kusanifisha Kiswahili. Madhumuni ya kamati hiyo ya lugha ilikuwa kama ifuatayo:
(a)
Kuendeleza
lugha moja kwa kupata maafikiano kamili katika mamlaka ya Afrika Mashariki.
(b)
Kuleta ulinganifu
kama itakavyoonekana, wa matumizi ya maneno yaliyoko na maneno mapya kwa
kusimamia uchapaji wa makamusi ya mashule na mengineyo.
(c)
Kuleta
ulinganifu wa sarufi kwa kuchapisha vitabu vya sarufi vilivyoafikiwa.
(d)
Kuwatia
moyo na kuwasaidia waandishi ambao ni
wenyeji wa lugha ya Kiswahili.
(e)
Kuandaa
vitabu vya Kiswahili vya kiada na vya ziada.
(f)
Kusahihisha
lugha ya vitabu vya shule na vinginevyo ambavyo vimechapishwa mara masahihisho
yanapohitajika.
(g)
Kutafsiri
kwa Kiswahili vile vitabu vilivyochaguliwa
kwa ajili ya kutumiwa shuleni au kwa kusoma kwa ziada au kuvitunga moja
kwa moja vitabu hivyo.
(h)
Kusoma na
kuhakiki vitabu vya Kiswahili vinavyoshughulikiwa na kamati.
(i)
Kuwapa
waandishi wa vitabu maelezo ya taratibu
za kufundishia za wakati uliopo katika nyanja mbalimbali.
(j)
Kujibu
maswali yoyote kuhusu lugha ya Kiswahili
na fasihi yake.
Kamati
hii ilitoa makamusi ya Standard
Swahili-English-Swahili Dictionary. Mwaka 1935 kulianzishwa mashindano ya
kuandika insha kwa Kiswahili katika shule za Kiafrika. Mwaka 1939 kukawa na
mashindano ya waandishi wa vitabu. Vile vile kamati ilitoa kijarida
kilichojulikana kwa jina la Bulletin of
the Inter-Territorial Language (Swahili) Committee.
(iii) Kutokana
na Vyombo Mbalimbali
Wakati
wa utawala wa Mwingereza vyombo vilivyosaidia sana kueneza Kiswahili ni:
(a) Elimu
Wakati
wa Mwingereza Kiswahili kilitumika kufundishia shule za msingi, darasa la
kwanza hadi la nne, na kilikuwa somo mojawapo hadi darasa la 12 katika shule za
Waafrika.
(b) Vyombo vya Habari
Vyombo
vya habari vilivyojishughulisha sana na kukuza na kueneza Kiswahili ni
magazeti, radio, nk.
·
Magazeti yaliyojishughulisha sana ni Masimulizi (1888), Habari za Mwezi (1894), Pwani
na Bara (1910), Rafiki Yangu
(1890), Habari za Leo (1954), Mwangaza (1923), Sauti ya Pwani (1940), Kiongozi
(1950), Mamboleo, nk.
·
Chombo kingine cha habari ni radio
Tanganyika ilianza matangazo kwa lugha ya Kiswahili mwaka 1950. Kwanza kama
Sauti ya D.S.M. halafu baadaye kama Sauti ya Tanganyika.
(c) Wakati wa Manamba
Utaratibu wa serikali za kikoloni ulikuwa ni kuzitenga sehemu fulani
kwa ajili ya vibarua wa kufanya kazi katika mashamba hayo, mawasiliano yote
yalifanywa kwa Kiswahili, na kwa njia hii kulikuwa na kukua na kuenea kwa
Kiswahili kwa urahisi zaidi hapa nchini.
(d) Suala la Jeshi (KAR)
Wanajeshi waliopigana katika vita mbalimbali walikuwa na nafasi ya
kusafiri sehemu mbalimbali na kwa kuwa lugha yao ya mawasiliano ilikuwa ni
Kiswahili, lugha hiyo iliweza kuenea kwa urahisi nchini.
(e) Kampeni za Kisiasa
Baada ya vita ya pili ya dunia, mataifa mengi yaliyokuwa yanatawaliwa
yalianza kudai uhuru wao, Afrika Mashariki nayo haikuwa nyuma.
Ingawa kulikuwa na makabila mengi yenye lugha tofauti, jambo
lililowauganisha ilikuwa ni lugha ya Kiswahili, ambayo iliweza kueleweka na
watu wengi. Lugha ya Kiswahili iliweza kuunganisha watu wa makabila tofauti
katika mikutano mbalimbali iliyokuwa ikifanywa na vyama vya siasa nchini wakati
huo.
No comments:
Post a Comment