Maana ya lugha
Lugha ni sauti za nasibu zilizo katika mpangilio maalumu na zilizo
kubaliwa na jamii ya watu zitumike kama chombo cha mawasiliano.
Au
Ni mfumo wa sauti za nasibu za kusemwa zinazotumiwa na watu wa jamii
fulani wenye utamaduni unaofanana kwa madhumuni ya mawasiliano katika
jamii hiyo.
Au
Katika kamusi ya Kiswahili sanifu TUKI 1981 oxford press uk. 86, inafafanua kuwa lugha ni mfumo wa sauti nasibu ambazo hutumiwa na jamii kwa madhumuni ya mawasiliano kati yao.
Sifa / tabia za lugha
Lugha huzaliwa
Lugha huzaliwa kutokana na mwingiliano kati ya lugha mbili au zaidi na
kutengeneza lugha moja. Kwa mfano lugha ya Kiswahili imetokana na
mwingiliano wa lugha mbalimbali za kibantu.
Lugha hukua
Lugha hukua kutokana na kuongezeka kwa msamiati mbalimbali ambayo
hutumiwa katika lugha husika katika shughuli mbalimbali. Msamiati
unapoongezeka katika lugha hiyo ni ishara ya hiyo lugha kukua.
Lugha huathiriwa
Jamii mbili tofauti zinazozungumza lugha mbili tofauti na zinapokaa
pamoja hakika zitaathiriana katika nyanja mabalimbali za kiutamaduni na
lugha ikiwemo. Athari hii katika lugha hasa huweza kujitokeza katika
matamshi, sarufi na hata lafudhi. Kwa mfano Kiswahili kimeathiri lugha
nyingi za kibantu ambapo mtu anaweza kuzungumza kilugha kwa Kiswahili
yaani mtu anaweza kuongea neno la lugha yake lakini akalitamka kwa
Kiswahili hali kadhalika Kiswahili pia kimeathiriwa na Kiingereza kwa
mfano mtu anaweza sema “Tafadhali nipe hilo daftari” msemaji huyu
atakuwa ameathiriwa na sarufi ya kiingereza ambapo kwa sarufi ya
Kiswahili ingefaa iwe “tafadhali naomba daftari hilo.”
Lugha hufa
Lugha hufa kutokana na kutotumika kwa lugha hiyo, endapo hiyo lugha
haitumiki kabisa basi msamiati hautaongezeka na hatimaye lugha hufa,
mfano mzuri nil lugha ya kilatini ambayo hivi sasa imebaki kwenye
maandishi tu, haizungumzwi tena, imekufa.
Lugha ina ubora
Kila lugha ni bora hakuna lugha iliyobora zaidi ya lugha nyingine, ubora
wa lugha unatokana na jinsi lugha hiyo inavyokidhi mahitaji ya
mawasiliano ya watumuaji wa lugha husika.
Lugha ni sauti za kusemwa na binadamu.
Tunapozungumzia lugha tunamaanisha sauti zinazosemwa na binadamu kinyume
na hapo ni ishara. Viumbe wengine wanatoa sauti lakini sio za kusemwa,
Mwanadamu hutumia alama za sauti kimsingi hakuna kiumbe ambacho si
binadamu kinachoweza kuzungumza lugha.
ASILI YA KISWAHILI
Neno asili kwa mujibu wa Massamba na wenzake (1999:3) ni jinsi kitu au
jambo lilivyotokea au lilivyoanza. Kutokana na fasili hii tunaona
kwamba jambo au kitu kinaweza kutokea kibahati kama ilivyo katika lugha
au linaweza kuanzishwa.
Hivyo basi asili ya lugha ya Kiswahili bado ni mjadala mrefu ambapo wataalamu mbalimbali wanahitilafiana juu ya asili au chimbuko la lugha ya kiswahili. Wapo wanaokinasibisha kiswahili na kiarabu kwa kutumia kigezo cha msamiati na dini ya kiislamu. Wengine wanashikilia msimamo kuwa kiswahili ni kibantu kwa kutumia hoja za kiisimu na kihistoria. Wapo wanaokinasibisha kiswahili na uchotara baadhi yao wanaoshikilia msimamo huu ni Freeman Grenville na Homo Sasson.
Kiswahili ni Kiarabu.
Hapa Kiswahili kimefasiliwa kuwa asili yake ni kiarabu, wanaoshikilia
mtazamo huu wanahoji kwamba katika lugha ya Kiswahili kuna maneno mengi
ya Kiarabu. Pia wanaeleza kuwa asili ya Kiswahili ni pwani na kwa kuwa
wenyeji wa pwani ni Waislamu na kwa kuwa uislamu uliletwa na Waarabu
basi hii lugha ya pwani nayo itakuwa imeletwa na Waarabu. Vigezo hivyo
vyote vina udhaifu mkubwa kwa sababu havikukitwa katika misingi ya
kitaalamu ya uainishaji lugha.
Kiswahili ni lugha Chotara
Mtazamo huu umezua ubishi mkubwa kwani hata baadhi ya wazawa
wamejinasibisha na uarabu na ushirazi. Wanaofasili Kiswahili kama lugha
chotara wanadai kuwa Kiswahili kimetokana na mchanganyiko wa lugha ya
Kiarabu na lugha za Kibantu. Hivyo Waswahili ni watu waliotokana na
wanaume wa Kiarabu na wanawake wa Kibantu.
Kiswahili ni lugha ya Vizalia
Waumini wa mtazamo huu wanadai kuwa Kiswahili kilianza kama pijini ya
Kiarabu na baadae kukomaa na kuwa kreoli. Pijini ni lugha ambayo
imetokana na mchanganyiko wa lugha mbili tofauti yaani Kiarabu na lugha
za Kibantu. Na kreoli ni lugha inayozungumzwa na watoto waliozaliwa na
baba Mwarabu na mama Mbantu.
Kiswahili ni Kikongo
Nadharia hii inafafanua kuwa lugha ya Kiswahili ilianzia huko Kongo na
kusambaa katika pwani ya Afika Mashariki. Wabatu walipofika Afrika
Mashariki waliingia kwa makundi na katika nyakati mbalibali. Makundi
hayo yalianza kujigawa na kutawanyika, matokeo ya kugawanyika huko ni
kutokea kwa makundi mbalimbali ya wabantu. Inasadikika kuwa baadhi ya
Wabantu walifanya maskani yao ya kudumu katika mabonde ya kaskazini mwa
mto tana. Kikundi hiki cha wabantu ndicho inasadikiwa kuwa chimbuko la
Kiswahili
Kiswahili ni Kibantu
Mtazamo huu ni ule unaoamini kuwa Kiswahili ni lugha ya Kibantu ambapo
lugha za Kibantu zilikuwepo hata kabla ya majilio ya wageni kutoka
Ajemi, Arabuni, India, China na kwingineko. Katika mtazamo huu lugha ya
Kiswahili inaingizwa katika kundi la lugha za Kibantu. Ama kwa hakika
mtazamo huu ulipata mashiko sana kuanzia karne ya ishirini, ulishadidiwa
kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na weledi wa isimu,
historia, akiolojia na ethnografia. Wanaisimu waliothibitisha kuwa
Kiswahili ni lugha ya Kibantu ni pamoja na Bleek (1862), Meinholf. C
(1932), Malcom Guthrie (1967, 1970, 1971), Doke (1935, 1945) na
wengineo. Vigezo vilivyotumika kufafanua kuwa Kiswahili ni kibantu ni
pamoja na:
- Msamiati
- Mofolojia
- Mfumo wa sauti
- Mfumo wa toni
- Mfumo wa ngeli
- Mpangilio wa maneno.
Ubantu wa Kiswahili: kigezo cha Kiisimu
Kigezo hiki cha kiisimu kimetumiwa na wataalam mbalimbali katika
kuonesha ubantu wa Kiswahili Massamba (1999) amewataja wataalam
mbalimbali ambao wamehusika na utafiti juu ya ubantu wa Kiswahili,
wataalam hao ni pamoja na Carl Meinhof katika kitabu chake cha Introduction to the phonology of the Bantu language, Duke
(1935 – 1945), Malcom Guthrie (1967), Dereck Nurse na Thomas Spear
(1985). Hawa walijadili ubantu wa Kiswahili kwa kutumia kigezo cha
kiisimu, kihistoria na kiakiolojia.
Katika kigezo cha kiisimu vipengele vinavyoangaliwa ni kama vile
kufanana kwa msamiati wa msingi, muundo wa kifonolojia, muundo wa
kimofolojia, muundo wa kisintaksia mpangilio wa ngeli za majina.
Mizizi ya msamiati wa msingi wa lugha za kibantu na Kiswahili hufanana kwa kiasi kikubwa, mifano ifuatayo huweza kuonesha ukweli huu.
Mfano,
Kiswahili
|
Kikurya
|
Kinyiha
|
Kijita
|
Maji
|
Amanche
|
Aminzi
|
Amanji
|
Jicho
|
Iriso
|
Iryinso
|
Eliso
|
Katika mifano hiyo hapo juu tunaona kuwa mizizi maji, manche, minzi,
manji inafanana kwa kiasi kikubwa, kwa hiyo huu ni ushahidi tosha
kutuonesha kuwa kuna uhusiano wa kinasaba kati ya Kiswahili na lugha za
kibantu.
Pia mofolojia ya Kiswahili na lugha za kibantu hufanana
kwa kiasi kikubwa, yaani mfumo wa maumbo ya maneno ya lugha ya
Kiswahili na lugha za kibatu hufanana. Kwa mfano, namna viambishi
vinavyopachikwa katika mzizi wa maneno hufuata kanuni ileile kama
inavyotumika katika lugha ya Kiswahili yaani viambishi vinaweza
kupachikwa kabla au baada ya mzizi na huwa na uamilifu bayana. Hebu
tuchunguze mifano ifuatayo:
Kiswahili
|
Kisukuma
|
Kisimbiti
|
Kinyiha
|
A-na-lim-a
|
a-le-lem-a
|
a-ra-rem-a
|
i-nku-lim-a
|
a-na-chek-a
|
A-le-sek-a
|
a-ra-sek-a
|
a-ku-sek-a
|
Kwa kuangalia mifano hii utagundua kwamba katika kutenganisha
viambishi hufuata kanuni moja kwamba mahali kinapokaa kiambishi kwa
mfano cha njeo, ndipo pia hukaa kwa upande wa lugha za kibantu, kwa
mfano –na- na –ra- katika lugha ya kisimbiti. Hivyo tunaweza kusema kuwa
kuna unasaba baina ya lugha hizi
Vilevile sintaksia ya lugha ya Kiswahili na lugha za kibantu hufanana kwa karibu sana. Kwa mfano jinsi ya mpangilio wa vipashio na kuunda sentensi hufanana
yaani mpangilio wa maneno hufuata kanuni maalum ambazo hufanana katika
Kiswahili na lugha za kibantu. Katika Kiswahili sentesi inakuwa na pande
mbili yaani upande wa kiima na upande wa kiarifu, katika upande wa
kiima kipashio chake kikuu ni nomino na katika upande wa kiarifu
kipashio chake kikuu ni kitenzi. Hii inamaana kwamba katika kuunda
sentensi ni lazima nomino ianze na baadaye kitenzi. Hebu tuangalie
mifano ifuatayo:
Kiswahili
|
Mama / anakula
N (K) T (A)
|
Kijita
|
Mai / kalya
N(K) T (A)
|
Kihehe
|
Mama/ ilya
N(K) T(A)
|
Kihaya
|
Mama / nalya
N(K) T(A)
|
Katika mifano hii tumeona kwamba muunndo wa kiima-kiarifu katika lugha
za kibantu unafanana sana na ule wa Kiswahili yaani nomino hukaa upande
wa kiima halikadhalika kitenzi hukaa upande wa kiarifu, kwa hiyo kwa
mifano hii tunaweza kusema kuwa lugha ya Kiswahili ni jamii ya lugha za
kibantu.
Pia mfumo wa sauti (fonolojia) wa
lugha za kibantu unafana sana na ule wa Kiswahili, yaani mpangilio wa
sauti katika kuunda silabi, na miundo ya silabi kwa ujumla hufanana. Kwa
mfano katika lugha ya Kiswahili hakuna muundo wa silabi funge yaani
silabi ambayo inaishia na konsonanti, muundo asilia wa silabi za
Kiswahili ni ule unaoishia na irabu vilevile katika lugha za kibantu
hufuata muundo wa silabi wazi, yaani silabi zote huishia na irabu.
Mifano ifuatayo hufafanua zaidi:
Kisawhili
|
Baba
|
K+I+K+I
|
Kikurya
|
Tata
|
K+I+K+I
|
Kiha
|
Data
|
K+I+K+I
|
Kijita
|
Rata
|
K+I+K+I
|
Kipare
|
Vava
|
K+I+K+I
|
Tanbihi: K= konsonanti I= irabu.
Kwa mifano hii tunaona kwamba mifumo ya sauti katika lugha za kibantu
hufanana na ule wa Kiswahili, kwa hiyo tunaweza kuhitimisha kwa kusema
kuwa lugha hizi ni za familia moja.
Pia vilevile mfumo wa ngeli za majina katika
lugha ya Kiswahili hufanana sana na ule wa kibantu hususani katika
upachikaji wa maumbo ya umoja na wingi na maumbo ya upatanisho wa
kisarufi. Katika lugha ya Kiswahili viambishi vya umoja na wingi
hupachikwa mwanzoni kabla ya mzizi wa neno, hivyohivyo katika lugha za
kibantu. Kwa mfano:
Umoja
|
Wingi
| |
Kiswahili
|
m-tu
|
wa-tu
|
Kikurya
|
mo-nto
|
abha-nto
|
Kiha
|
umu-ntu
|
abha-ntu
|
Kikwaya
|
mu-nu
|
abha-nu
|
Mifano hiyo hapo juu inadhihirisha wazi kwamba vipashio vyote vya umoja
na wingi hujitokeza kabla ya mzizi wa neno, hivyo ni dhahiri lugha hizi
zina uhusiano wa nasaba moja.
Vilevile katika upatanisho wa kisarufi lugha za kibantu na Kiswahili huelekea kufanana viambishi vya upatanisho wa kisarufi hususani viambisha vya nafsi.
Kwa mfano:
Kiswahili
|
Mtoto a-nalia
|
Kizanaki
|
Umwana a-rarira
|
Kisukuma
|
Ng’wana a-lelela
|
Kikurya
|
Omona a-rakura
|
Tunaona hapo juu kwamba kiambishi ‘a’ cha upatanisho wa kisarufi
hujitokeza katika lugha zote, hivyo tunashawishika kusema kuwa Kiswahili
kina uhusiano mkubwa na kibantu.
Pamoja na ushahidi wa kiisimu kutupatia vithibitisho tosha juu ya ubantu
wa Kiswahili pia kuna ushahidi mwingine kama vile ushahidi wa
kihistoria, kiakiolojia na kiethinolojia.
Ushahidi wa Kihistoria
Ushahidi wa kihistoria huchunguza masimulizi na vitabu mbalimbali vya
kale ambavyo huelezea asili na chimbuko la wakazi wa upwa wa Afrika
Mashariki. Vilevile ugunduzi wa kiakiolojia huonesha kuwa kulikuwa na
wakazi wa asili wa upwa wa Afrika Mashariki ambao walikuwa na utamaduni
wao na maendeleo yao hata kabla ya kuja kwa wageni. Katika ushahidi wa
kiethinolojia, huchunguzwa tarihi mbalimbali zinazojaribu kutoa historia
ya watu wa pwani ya Afrika Mashariki na lugha yao.
Kwa ujumla vyanzo hivi vyote huonesha kuwa pwani ya Afrika mashariki
ilikuwa na wakazi wake wa asili ambao walikuwa na lugha yao, utamaduni
wao na pia maendeleo yao, vyanzo hivi pia huhitimisha kwa kusema kuwa
lugha ya wakazi hawa ilikuwa ni Kiswahili.
Kukua na kuenea kwa kiswahili wakati wa ukoloni
Katika
karne ya kumi na tisa Afrika Mashariki iliingia kwenye mahusiano na
mataifa mengine kama vile Marekani, Ujerumani na Uingereza. Mahusiano
haya ni baada ya watu wa pwani kuwa na uhusiano wa muda mrefu wa
kibiashara na Waaarabu, hawa waliweka athari kubwa katika kukua na
kuenea kwa lugha ya Kiswahili. Wageni kutoka Ulaya walipoingia Afrika
Mashariki walifanya biashara, shughuli za kidini (mishenari), elimu na
utawala. Kama ilivyokuwa katika kipindi cha Waarabu, uwepo wao pia
ulikuwa na athari katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili Afrika
Mashariki na kwingineko.
Maendeleo ya Kiswahili kipindi cha waarabu
Waarabu hasa katika pwani ya Afrika Mashariki walifanya biashara ikiwemo
biashara ya watumwa. Ilikuwepo misafara mbalimbali ya biashara kutoka
pwani hadi bara. Katika misafara hiyo Kiswahili ndio ilikuwa lugha ya
mawasiliano hivyo Kiswahili kikaenea pia katika sehemu za bara.
Kuna mambo kadhaa waliyofanya waarabu ambayo yalichangia kukua kwa lugha
ya Kiswahili. Waarabu walichangia kukua kwa lugha ya Kiswahili kama
ifuatavyo:
Biashara
Waarabu walifanya biashara kati ya pwani na sehemu za bara, katika
biashara yao walichangia kwa kiasi kikubwa uenezaji wa lugha ya
Kiswahili. Lugha kuu ya mawasiliano na ya kibiashara iliyotumiwa na
wafanya biashara wa kiarabu ilikuwa ni Kiswahili, kwa hiyo kwa njia hii
waliweza kueneza Kiswahili kuanzia pwani hadi maeneo ya bara kama vile
Tabora, Kigoma hadi mashariki mwa Kongo.
Dini
Dini pia ni jambo ambalo liliweza kuchangia ueneaji wa lugha ya
Kiswahili enzi za waarabu. Waarabu walipokuja walitaka kueneza dini yao
kwa undani kabisa. Kwa hivyo iliwabidi kuanzisha madarasa ambayo
walitumia kufundishia, lugha iliyokuwa ikitumiwa ni lugha ya Kiswahili.
Na hivyo hii ikasaidia kuenea kwa lugha ya Kiswahili.
Maandishi ya kiarabu
Waarabu pia walileta hati zao zilizotumiwa katika maandishi ya lugha ya
Kiswahili. Kwa hiyo kupitia hati za kiarabu maandishi mbalimbali ya
lugha ya Kiswahili yaliweza kuhifadhiwa, hivyo Kiswahili kiliweza kukua
kwa vile kingeweza kuhifadhiwa katika maandishi na kusomwa wakati
wowote.
Kuoana
Pia vilevile Waarabu waliofika pwani waliweza kuoana na wabantu, hii
ilisababisha kizazi kipya kutokea. Na kwa sababu hiyo watoto
walichukua maneno mengi kutoka kwa baba na mama yao na hivyo kuongeza
msamiati katika lugha Kiswahili.
Maendeleo ya Kiswahili kipindi cha wajerumani
Wajerumani waliingia katika pwani ya Afrika Mashariki katika miaka ya
1875, walifanya kila jitihada kuwatawala Waafrika ambapo katika utawala
wao walifanya biashara, waliendesha shughuli za kiutawala, za kidini na
kielimu. Katika shuguli zote hizo Kiswahili ndio ilikuwa lugha ya
mawasilino hivyo kukikuza na kukiendeleza Kiswahili.
Walipongia katika pwani ya Afrika Mashariki walikuta Kiswahili
kimekwisha enea kwa kiasi kikubwa. Kuna mambo waliyoyafanya ambayo
yalisaidia kukua na kuenea kwa Kiswahili kama ifuatavyo:
Kutoa mafunzo ya lazima ya lugha ya Kiswahili kwa wafanya kazi wa serikali
Waliwalazimisha wafaanyikazi wote wa serikali kujifunza kiswashili, kwa
sababu sheria ilikuwa ni kwamba pasipojua Kiswahili huwezijiriwa katika
serekali ya mjerumani. Kwa hiyo saula hili lilisababisha watu kujifunza
lugha ya Kiswahili ili waweze kuajiriwa. Wafanyakazi ambao ilikuwa ni
lazima wajifuze Kiswahili ni pamona na maakida.
Wajerumani wenyewe walilazimika kujifunza kiswahili ili waweze
kuwasiliana na wenyeji kwa urahisi na hivyo kurahisisha shuguli zao za
kiutawala.
Ujenzi wa shule
Shule zilifunguliwa kufundisha watu weusi ili waje wawe wasidizi wao
katika utawala wa wajerumani, na lugha iliyokuwa ikitumika kufundisha
masomo ilikuwa ni lugha ya Kiswahili.
Kuenea kwa utawala wa Wajerumani nchi nzima
Utawala wa wajerumani ulikuwa kwenye kila kona ya nchi. Na kwa kuwa
wafanya kazi wa serikali ya wakati huo ilikuwa ni lazima wafahamu
Kiswahili, kwa hiyo kila sehemu palipokuwa na ofisi za serikali nchi
nzima kulizungumzwa Kiswahili.
Shughuli za kiuchumi
Pia katika shuguli za mashamba, wajerumani walichukua vibarua kutoka
sehemu mbalimbali za nchi, na kwa kuwa kila mmoja alikuwa na lugha yake
tofauti, kwa hiyo lugha pekee iliyowaunganisha katika mawasiliano kwenye
eneo la kazi ilikuwa ni Kiswahili.
Kwa hiyo kutokana na sababu kwamba utawala wa kijerumani ulitoa msukumo
mkubwa katika matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye shughuli zao za
kiutawala, hivyo suala la ueneaji wa Kiswahili lisingeepukika.
No comments:
Post a Comment